TAA yaita wawekezaji viwanja vya ndege

 

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), imewataka Watanzania kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji zilizopo katika viwanja vya ndege nchini, huku akibainisha kuwa viwanja vya ndege sio tu kwa ajili ya kusafiri, ila shughuli nyingine za kijamii, kiuchumi na uzalishaji zinaweza kufanyika.

Hayo yamesemwa leo Mkurugenzi wa wa TAA, Fedha Shadrack Chilongani, aliyemwakilisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, na kueleza kuwa wameshiriki Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), maalum kwa ajili ya kuwaeleza wananchi shughuli zinazofanywa na TAA sambamba na fursa zilizopo.

“Katika viwanja vyetu, unaweza ukawekeza kujenga mahoteli, kumbi za mikutano, vituo vya kujaza mafuta, migahawa na fursa nyingine,” amesema kiongozi huyo.

Amesema, Watanzania wanapaswa kufahamu kuwa katika eneo la usafiri wa anga kuna mamlaka mbalimbali ambazo zinafanyakazi kwa kutegemeana, ingawa kila moja ina majukumu yake.

Ametolea mfano wa TAA ambayo wana wajibu wa kusimamia na kuboresha viwanja 59 vya ndege, kati ya hivyo, viwanja 14 vina miundombinu thabiti ya uwekezaji kama lami na miundombinu mingine wezeshi.

“Viwanja vyenye miundombinu ya taa ni 8, tayari vinatumika kwa safari za usiku,” amesema kiongozi huyo na kutanabahisha kuwa TAA wanashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), pia Shirika la Ndege nchini (ATCL), ili kuhakikisha huduma za usafiri wa ndege zinatekelezeka ipasavyo.
Previous Post Next Post