Yanga inabeba tena
Samson Mbangula anaumaliza msimu wa Simba katika Ligi Kuu Bara kirahisi pale Jamhuri, Morogoro.
Mabao yake mawili ni kilio kipya Msimbazi kwa kuzima ndoto za kuwania ubingwa msimu huu. Kipigo kizito. Kipigo cha maumivu kwa Wanasimba wote.

Ushindi wa Tanzania Prisons mbele ya Simba pale Morogoro ni kama mpasuko mkubwa katika jahazi lililo katikati ya Bahari. Imeziweka hesabu za Simba kuwania ubingwa msimu huu kuwa ngumu kabisa.
Simba hata ikishinda mchezo wa kiporo dhidi ya Mtibwa Sugar bado itakuwa imeachwa alama saba na Yanga. Ni alama nyingi mwa Mnyama kuweza kuzifikia. Hesabu ni ngumu sana kwa Simba.

Unaweza kuona kuwa alama saba sio nyingi, ila kiwango cha Simba kwenye ligi kinafanya zionekane nyingi sana. Simba hawana uhakika wa kushinda mechi tano mfululizo
Simba haina uhakika wa kushinda mechi za dabi dhidi ya Azam FC na Yanga. Hivyo uwezekano wa wigo huo wa alama kuongezeka ni rahisi zaidi kuliko kupungua.

Kiwango cha sasa cha Yanga ni vigumu kuzuilika. Yanga ipo kwenye ubora wa juu sana. Inashinda kila mechi. Tangu kurejea kwa Ligi Kuu mapema Februari, Yanga imepata sare moja tu.
Iwe inawakosa wachezaji wengi muhimu ama la, bado Yanga itakiwasha. Nani ataizuia Yanga kwa siku za karibuni? Hakuna. Yanga ipo kwenye kilele cha ubora wake.


Wachezaji wengi wa Yanga wapo kwenye ubora wao. Kocha Miguel Gamondi yupo kwenye kilele cha mbinu zake. Yanga inavyocheza kipindi cha kwanza ni tofauti kabisa na cha pili. Wanakuwa wa moto kadri muda unavyokwenda uwanjani.

Kiwango hiki cha Yanga ndio kinaniaminisha kuwa kwa msimu huu ni ngumu tena kuwazuia. Wameweka biashara yao vizuri na sasa wanakwenda kutwaa taji la tatu mfululizo.

Pengine ungetegemea ushindani kutoka kwa Azam, lakini nao wameendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu. Walikuwa kwenye kiwango bora kabla ya Ligi kusimama. Wamerejea wako hoi. Wamepoteza alama nyingi kizembe. Kwa sasa hawako kabisa kwenye njia ya ubingwa.

Miaka yote Azam imekuwa hivyo. Inapopewa nafasi ya kukimbizana kwenye ubingwa ndio inapoteana kabisa. Msimu huu ina wachezaji wazuri, lakini bado imeshindwa kuwa na ushindani mkubwa.
Kwa hesabu za ubingwa kuibeba Yanga kwa sasa, ni wazi kuwa Simba wanahitaji kurejea katika kioo na kujitazama upya. Wanakosea wapi? Wanakwama wapi? Wafanye nini kujikwamua?

Ni maswali ambayo wanapaswa kuyajibu mapema kabisa wakienda kujipanga kwaajili ya msimu ujao. Vinginevyo watashuhudia Yanga ikibeba ubingwa wa nne mfululizo.

Kwanza eneo la usajili Simba inapaswa kulifanyia kazi vizuri sana. Pengine wanaohusika kutafuta wachezaji hawajui wanachokifanya ama timu ina bajeti ndogo ya kununua mastaa.

Pengine waliopewa kazi hiyo hawafahamu namna ya kupata wachezaji wazuri. Hii ndio sababu nyoa wengi waliotua Simba wamekua na viwango vya kawaida. Inafikirisha sana.

Cha pili ni katika eneo la usimamizi wa timu. Wachezaji wa Simba ni kama vile wamekuwa wakubwa sana. Utawakuta viwanja wanazurura usiku wakati huu ratiba ya Ligi ni ngumu.

Nimewaona maeneo mengi usiku. Ni wazi kuwa wanatoroka kambini. Nani anapaswa kuwadhibiti? Ni eneo ambalo linahitaji maboresho.

Eneo la kutathmini mechi linapaswa kufanyiwa kazi. Nani anatazama video za Simba na kuzifanyia tathmini kisha kumpatia kocha? Nani anatazama video za timu pinzani na kuzifanyia kazi kisha kumpatia kocha. Ni wazi kuwa wanaofanya kazi katika eneo hili kuna mahali wamefeli.

Mechi nyingi utakuta Simba inafanya makosa yale yale. Utakuta mechi nyingi Simba inaonekana kuwa haikuwasoma wapinzani. Kwanini wakati watu wa video wapo? Ni wazi kunahitaji maboresho.
Yote kwa yote ubingwa umekaa mkao kwa Yanga. Sasa Simba waanze mipango ya msimu ujao mapema.

Hili la Dube ni kituko kingine Bara

STRAIKA raia wa Zimbabwe, Prince Dube amepeleka maombi ya kuvunja mkataba Azam FC. Ni ghafla sana. Imekuwa mshtuko mkubwa. Dube ni miongoni mwa nembo za Azam. Amejipambanua kuwa mchezaji mahiri pale Chamazi.

Licha ya majeraha ya mara kwa mara, Dube amekuwa miongoni wa wachezaji waliofanya vyema Azam katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyopita.
Kwa nini anaondoka? Ni swali gumu sana. Ila kwa maelezo yake, anataka changamoto mpya. Pengine anataka kushinda mataji pia. Ameona Azam hawawezi kumpa.
Kinachofikirisha kwenye hili la Dube ni kwa nini atake kuondoka wakati huu ambao dirisha la usajili limefungwa? Kwa nini asingesubiri msimu umalizike? Inafikirisha sana.

Kinachoshangaza zaidi ni baadhi ya watu kuona Dube ana haki ya kuvunja mkataba kinyemela.

Azam wameweka wazi hawana shida na Dube. Kama anataka kuvunja mkataba aweke kiasi cha fedha kama walivyokubaliana. Ni Dola 300,000.
Ni fedha nyingi sana. Ni zaidi ya Sh750 milioni. Wamemwambia alipe fedha hizo kisha aondoke zake. Ndio mkataba wake unasema hivyo.

Ni kama Fei Toto alivyowalipa Yanga wakati ule. Bahati mbaya ni kwamba Yanga waliweka fedha kidogo kwenye kipengele hicho, Azam wameweka nyingi. Ndio utofauti.

Utofauti mwingine ni Yanga walikataa kulipwa fedha hizo, ila Azam wamekubali. Ila kituko ni kwamba watu wanataka Azam wamruhusu Dube aondoke bure.
Previous Post Next Post