Robo fainali si habari tena, njia ya nusu ni hii

 

JUZI Jumamosi, Simba ilihitimisha kuandikwa kwa historia ya soka Tanzania wakati ilipofuzu kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuiwezesha nchi kuingiza timu mbili katika hatua hiyo kwa mara ya kwanza.

Simba iliishinda Jwaneng Galaxy ya Botswana kwa mabao 6-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika moja ya mechi za mwisho za Kundi B na kuungana na Asec Mimosas ya Ivory Coast kusonga mbele kwenda hatua ya tatu ya juu kwenye mashindano hayo, licha ya kufungwa bao 1-0 ugenini na Wydad CA ya Morocco.

Yanga ilishafuzu tangu wiki moja iliyopita baada ya kuitandika CR Belouizdad ya Algeria kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Mkapa, hivyo kuungana na Al Ahly ya Misri kuingia robo fainali kutoka Kundi D.

Hayo ni mafanikio makubwa katika soka la Tanzania ambalo kimataifa limezidi kung’ara kulikochangiwa na uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuruhusu idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni ambao wameonyesha uwezo wa kupambana na wachezaji kutoka Afrika Kaskazini na Magharibi.

Hii si hatua ngeni kwa klabu zote mbili baada ya Yanga kufuzu mwaka 1998 wakati mfumo mpya wa mashindano ya klabu bingwa ya Afrika ulipoanza. Wakati huo, robo fainali ilichezwa kwa makundi na Yanga ilimaliza mkiani mwa kundi B ililopangwa na Manning Rangers ya Afrika Kusini, Raja Casablanca ya Morocco na Asec ya Ivory Coast.

Simba ndio imejenga mazoea ya kufika hatua hiyo kutokana na mafanikio ya miaka mitano iliyopita. Hii ni mara ya tano kwa Simba kufuzu kucheza robo fainali katika mfumo huu mpya tangu ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 2003.

Changamoto kubwa kwa Simba imekuwa ni kuvuka kwenda hatua ya nusu fainali ambako mara nyingi kuna vigogo kutoka Afrika Kaskazini, na siku hizi timu za Afrika Kusini kama Orlando Pirates, Kaizer Chiefs na wababe wa Afrika, Mamelodi Sundowns ambao wanashikilia ubingwa wa mashindano mapya ya Ligi ya Soka Afrika (AFL).

Tangu ilipofuzu mwaka 1998 na kushika mkia kwenye kundi, Yanga haikuwahi kufikia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, hivyo kufikia robo fainali ni ziada ya matarajio yao waliyoyaeleza tangu mwanzoni kuwa malengo yao ni kufuzu kucheza makundi baada ya vigogo hao wa Jangwani kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana waliposhindwa na USM Alger kwa sheria ya bao la ugenini.

Hivi sasa vigogo wote hao, wako robo fainali ambako wanatarajia kukutana na timu ngumu. Wawakilishi hao wa Tanzania walioshika nafasi ya pili katika makundi yao, sasa wanaweza kukutana na ama Asec Mimosas, Mamelodi Sundowns au Petro Atletico ya Angola pamoja na Al Ahly ya Misri ambao ni mabingwa watetezi.

Na hapo ndipo penye habari kubwa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika kwa soka la Tanzania.  Karibu mara nne ambazo Simba ilifika robo fainali, ilionekana kama ingeweza kuvunja mwiko na kutinga nusu, lakini mikakati mibovu ya kucheza ugenini iliigharimu.

Mara zote haikuwa inaheshimu wapinzani wanapokuwa nyumbani, makocha wake wakitaka kucheza kwa kushambulia kutoka mwanzo wa mchezo hadi mwisho na kujikuta ikiruhusu rundo la mabao ambayo haikuwa rahisi kuyarejesha nyumbani.

Mfano mzuri ni mechi dhidi ya Orlando Pirates. Katika mechi ya kwanza Afrika Kusini, Simba ilicheza soka la kushambulia tangu mwanzo.

Hata iliporuhusu bao la kwanza, iliendelea kushambulia. Ikaruhusu la pili, la tatu na la nne na hivyo kumaliza mchezo ikifungwa mabao 4-0 ambayo yalikuwa mlima mrefu kwa wababe hao wa Mtaa wa Msimbazi.

Orlando walipokuja nchini walishambulia kwa dakika 20 za mwanzo na baadaye kurudi nyuma kujilinda, ikifanya mashambulizi ya kushtukiza. Simba ilifanikiwa kufunga mabao 3-0 na hivyo kutolewa.

Lakini hali imebadilika kwa timu zote. Simba ilianza vibaya mashindano ya mwaka huu, ikiwa imemtimua kocha mkuu, Roberto Oliveira 'Robertinho' na hivyo Abdelhak Benchikha kuwa na wakati mgumu wa kuitengeneza tena timu kwa falsafa zake na angalau sasa inaonekana kuanza kuimarika.

Yanga imekuwa na mwenendo mzuri tangu mwanzo wa michuano hii, ikipata ushindi pale ambapo haikutegemewa na ikavuka kwenda robo fainali kwa kishindo baada ya kuishinda CR Belouizdad kwa mabao 4-0, ukiwa ni ushindi wa kwanza mkubwa dhidi ya timu kutoka Afrika ya Kaskazini.

Lakini haya yatabakia kuwa ya kawaida iwapo wawakilishi hao wa Tanzania watagotea tena robo fainali. Hakutakuwa na jipya zaidi ya mashabiki kudhihakiana na kuchekana mitandaoni na kwenye vijiwe.

Kuna watakaowacheka sana wengine, lakini hiyo haitakuwa faraja kwa soka la Tanzania kwa kuwa mwisho wa kicheko itakuwa ni kulilia maumivu ya kutovuka hatua ya robo fainali kulikoibua jina la utani la ‘Mwakarobo’.

Ni wakati sasa wa kujipanga kiufundi zaidi wakati wa kujiandaa kwa mechi za robo fainali. Kama ule utamaduni wetu wa kuomba kuahirishiwa mechi za ligi ya ndani ili tujiandae kimataifa haujaweza kutusaidia kuvuka robo, basi tuachane nao.


Kama ule utamaduni wetu wa kung’ang’ania wachezaji wale wale kwenye mechi za Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la Azam na Ligi ya Mabingwa haujatusaidia, hebu tuanze kuwapumzisha na kuwapa nafasi kina Ladack Chasambi na Denis Nkane wapashe miili kujenga afya ya timu.

Kuna mambo mengi ambayo tumezoea kuyafanya wakati tukijiandaa kwa mechi za kimataifa, lakini hayajatusaidia. Ni lazima tuyatathmini na kuachana nayo kama ni lazima ili tuingie kwa nguvu tofauti katika mechi za robo fainali na tuimarishe mafanikio haya ya kuingiza timu mbili hatua hiyo kwa kuzipeleka zote nusu fainali kama ikiwezekana.


Previous Post Next Post