Soko la madini lahitajika haraka Tunduru

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro ameagiza kukamilishwa ujenzi wa soko la kisasa la madini ya vito litakalokuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki.

Soko hilo linajengwa katika Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kusaidia kukomesha mianya ya utoroshaji wa madini.
Agizo hilo amelitoa leo Jumatatu Machi 4, 2024 baada ya kutembelea ujenzi wa soko hilo akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Mtatiro amesema amefurahishwa na hatua za ujenzi huo, anaosema una tija kwa mustakabali wa rasilimali za Tanzania.

"Naelekeza uongozi wa Halmashauri ya Tunduru kukamilisha haraka ujenzi wa soko hili la kisasa la madini ya vito na lianze kufanya kazi kwa wakati,” amesema mkuu huyo wa wilaya Mtatiro.

Amesema likianza litasaidia kupunguza kama si kumaliza vitendo vya utoroshaji wa madini ya vito wilayani humo.

Amaesema utoroshaji huo unafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao wanasababisha Serikali kukosa mapato na kodi.

Amefafanua zaidi kuwa, soko hilo likianza Serikali haitaruhusu tena masoko madogo madogo aliyosema ni chanzo cha utoroshaji wa madini nje ya masoko.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Chiza Marando alisema ujenzi huo ulioanza mwishoni mwa Desemba 2023, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi ujao na utagharimu Sh1.087 bilioni na jengo hilo litakuwa na uwezo wa kutumiwa na kampuni 155 za madini ya vito kwa wakati mmoja.

Marando amesema zaidi ya kampuni 130 zimeshaomba nafasi ya kufanyia biashara kwenye soko hilo .

“Kampuni za madini ambazo zinafanya kazi kwenye masoko madogo madogo ya madini wilayani hapa zijiandae kuhamia kwenye soko la pamoja la kimataifa k,” amesema.

Ofisa Migodi wa Wilaya ya Tunduru Emmanuel Bushi ameeleza kuwa soko jipya la pamoja ni mkombozi wa wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya vito wilayani humo kwa kuwa watapata ushindani na bei zenye tija kuliko hivyo sasa.
Previous Post Next Post